#National Affairs
Target:
Tanzanian citizens
Region:
Tanzania
Website:
www.bongotz.com

Lengo letu ni kukusanya sahihi zipatazo milioni moja na kuziwakilisha kwa Rais Kikwete tukiitaka serikali iwekeze kwenye mradi wa Stieglers Gorge, uliopo kwenye bonde la mto Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawatt 2100 [mwingi wa kutosha na hata mwingine kubaki na kuuzwa nje ya nchi] ili tuweze kuondokana kabisa na tatizo hili la kukatikiwa na umeme, tatizo ambalo ni aibu kubwa kwa taifa letu.

Stieglers Gorge ni nini hasa? Stieglers Gorge ni mpalio mwembaba unaopatikana kwenye bonde la mto Rufiji, kilomita 374 toka jijini Dar es salaam. Kwa utafiti uliowahi kufanyika mwishoni mwa miaka ya sabini na mwanzoni mwa miaka ya themanini [ 1978-1980] kwa ushirikiano wa RUBADA [Rufiji Basin Development Authority] na M/s Norplan/Hafslund, ilionekana kwamba mradi wa Stieglers Gorge una uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme mwingi kwa njia ya maji [Hdro-power] zaidi ya umeme ambao Tanzania ilikuwa ikihitaji katika miaka hiyo. Matokeo ya utafiti huo pia yalionyesha kwamba, mpalio wa Stieglers una uwezo wa kuhimili mitambo mitatu mikubwa ya kuzalisha umeme [3 power stations]. Mtambo 'A' wenye uwezo wa kuzalisha megawati mia nne (400MW) ambao ungefungwa upande wa kaskazini mwa bwawa. Mtambo 'B' wenye uwezo wa kuzalisha megawati mia nane (800MW) ambao ungefungwa upande chini ya bwawa, na mtambo 'C' wenye uwezo wa kuzalisha megawati mia tisa (900MW) ambao ungefungwa upande wa kusini mwa bwawa. Jumla megawati elfu mbili mia moja [2100MW].

Ilikadiriwa kwamba, kwa kipindi hicho [1978-1980], ingeigharimu serikali dola milioni 1,200 za kimarekani tu kukamilisha mradi wote.

Lakini cha kushangaza, kwa sababu zisizoeleweka, serikali ikaamua kutoendelea na mradi huu na badala yake ikaamua kuwekeza kwenye vijimradi vidogovidogo kama vile Hale, Mtera, na Nyumba ya Mungu. Matokeo yake, sina haja ya kuyaelezea.

Ndugu watanzania wenzangu, wajibu wa hatma ya nchi yetu umo mikononi mwetu sote. Mustakabali wa taifa letu hautategemea viongozi waoga toka serikali kuu wanaong'ang'ania dhana ya "status quo" kwa kutopenda kujaribu mambo mapya na makubwa ya kimaendeleo. Maendeleo ya kweli hata hivyo, yataletwa na sisi wenyewe, wananchi.

Kwasababu hiyo basi, BongoTz kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi tumeamua kuanzisha movement ya kuishinikiza serikali kutafuta suluhu ya kuridhisha na ya kudumu kuhusu tatizo la umeme/nishati nchini.

Lengo letu ni kukusanya sahihi zipatazo milioni moja na kuziwakilisha kwa Rais Kikwete tukiitaka serikali iwekeze kwenye mradi wa Stieglers Gorge, uliopo kwenye bonde la mto Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawatt 2100 [mwingi wa kutosha na hata mwingine kubaki na kuuzwa nje ya nchi] ili tuweze kuondokana kabisa na tatizo hili la kukatikiwa na umeme, tatizo ambalo ni aibu kubwa kwa taifa letu.

Haileti maana kabisa kwa nchi yetu iliyobarikiwa kwa vyanzo vingi vya kuzalisha umeme kama vile makaa ya mawe--Mchuchuma na Kiwira; gesi ya asili "songo songo"--ufukweni mwa bahari ya Hindi na Mnazi bay (Mtwara); pamoja na chanzo kingine rahisi kwa njia ya maji [Hydro-power]--Stieglers Gorge, Rufiji; kuendelea kusuasua kwenye kiza kinene miaka nenda, miaka rudi.

Sio kwamba Rais wetu halijui hili, hapana, analijua fika! Yeye mwenyewe, kwenye ufunguzi wa Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 30 desemba 2005 alitamka na kuahidi mbele ya wabunge, nanukuu: "Nishati ni sawa na chembe za damu mwilini. Tunapanua wigo na aina ya vyanzo vya umeme na nishati kwa jumla ili kuwa na nishati ya kutosha na yenye gharama nafuu kukidhi mahitaji ya uzalishaji ya viwanda, utoaji wa huduma za kijamii, na matumizi ya nyumbani. Tutayashughulikia kwa kipaumbele cha juu matatizo ya sasa yahusuyo upatikanaji wa umeme nchini... Ilani ya CCM ya uchaguzi wa Oktoba 2005 inasema wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne itaharakisha mradi wa kupata umeme kutoka makaa ya mawe ya Mchuchuma. Na Hivyo ndivyo tutakavyofanya. Aidha, Serikali ya Awamu ya Nne itafufua miradi ya umeme ya mto Rusomo na Stiglers [Stieglers Gorge]." Mwisho wa kunukuu..

Ndugu watanzania wenzangu popote pale mlipo: ushirikiano wetu sote unahitajika ili kufanikisha zoezi hili. Tafadhali sign petition hapo chini kisha wafahamishe na wengine pia. Maana tusiposhiriki sasa, nani ajuaye kesho watatuletea hadithi gani tena? Juzi ilikuwa IPTL na Richmond. Jana ilikuwa kununua mvua toka Thailand, wakati Stieglers Gorge ipo. Na kesho je...?

Yes, viongozi wetu kwasasa wanaweza kujidai kuziba masikio wasitake kusikia kilio chetu kama walivyozoea sikuzote, lakini tukumbuke kuwa sahihi 25,000 za wanaharakati wa Seberia wakiongozwa na mwana-biolojia Marina Rhikhvanova ziliilazimu serikali ya Kremlin kusitisha mpango wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta karibu na ziwa Baikal, ziwa lenye kina kirefu duniani. Je, itakuweje kwa sahihi milioni moja toka kwa watanzania wenye uchungu na nchi yao?

GoPetition respects your privacy.

The TATIZO LA UMEME: TUPATIENI 'STIEGLERS GORGE' petition to Tanzanian citizens was written by BongoTz and is in the category National Affairs at GoPetition.